WAZIRI MKUU MAJALIWA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA MAENEO YA KILIMO KWA VIJANA




Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim M. Majaliwa amezitaka Halmashauri nchini kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana ili kuwavutia vijana kushiriki kwenye kilimo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya  wakati wa uzinduzi wa Progamu ya Vijana ya “JENGA KESHO BORA KWA VIJANA” inayosimamiwa na  Wizara ya Kilimo iliyoenda sambamba na Programu ya FARM CLINIC inayosimamiwa na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na Kampuni ya Mwananchi Communications na VODACOM TANZANIA.

“Nawapongeza Wizara kwa kuja na ubunifu mkubwa wa kuwafikia vijana wengi nchini Tanzania katika kuhakikisha kundi hili kubwa linashiriki kikamilifu kwenye sekta ya Kilimo.

Mh.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa sekta hii ameongeza Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa kiwango kikubwa sana ili miradi mingi itekelezeke kwa urahisi na haraka kwa kutambua kwamba sekta hii ni mwajiri mkuu na inatoa mchango mkubwa wa kupunguza changamoto ya Ajira hasa kwa vijana.


Naziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha mnatenga maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo ili kuwe na wigo mpana wa ushiriki wa Vijana katika maeneo yote,wakati huo huo Vijana hakikisheni mnaichangamkia hii fursa ya kilimo ili kutatua pia changamoto ya ajira”Alisema Waziri Mkuu Majaliwa

Akitoa maelezo ya awali,Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde amesema katika Programu hii ya Vijana Serikali itatafuta maeneo ya kilimo na itayasafisha,itapima afya ya udongo,itaweka miundombinu muhimu ya kilimo cha umwagiliaji,itagawa pembejeo na kuwatafutia masoko vijana,ambapo mpaka sasa jumla ya zaidi ya ekari 69,000 zimetengwa katika mikoa ya Dodoma na Mbeya kwa ajili ya mashamba makubwa ya pamoja(Block farms) na itarajiwa zaidi ya ajira milioni tatu zitazalishwa kupitia programu hii.

Comments