TRAFIKI WENGI BARABARANI - KINANA



Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinanana amemshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura kufanya tathimini ili kuona uwezekano wa kupunguza idadi ya Askari wa usalama barabarani ambao wanalalamikiwa na Wananchi kusababisha kero.

Kinana ametoa ushauri huo jana akiwa katika mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Songwe na Mbeya wamelalamikia idadi kubwa ya Askari wa barabarani ambao wamekuwa wakiwasimamisha mara kwa mara, kutaka fedha ambazo hata hivyo hawatoi stakabadhi yoyote.

Malalamiko hayo ya Wananchi yaliendelea kuibuka hata katika kikao cha ndani cha Wanachama wa CCM Mkoa wa Songwe ambapo mmoja ya wanachama hao, dereva wa magari ya kubeba abiria, ametoa malalamiko mbele ya Kinana akidai wamechoka kusimamishwa mara kwa mara na Trafiki na kila wanaposimama wanatoa sh. 2,000 kwa kila kituo.

Akijibu malalamiko hayo Kinana amesema “Nampongeza Rais kwa kumtea IGP mpya, nina hakika ni IGP mwadilifu, mchapakazi na hodari lakini namuomba na kumshauri atazame wingi wa Trafiki mijini, kila baada ya muda mfupi unasimamishwa na Trafiku, wenye magari hawaendeshi kwa raha, hivyo nimsihi IGP afanye tathimini kuhusu uwepo wa Trafiki wengi kwenye miji yetu, wamekuwa wengi sana kila ukitembea kidogo unasimamishwa, kilomita moja unakuta Trafiki”

Comments