Aweso ataka bei elekezi kuunganisha maji nchini
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameziagiza mamlaka za maji kuwa na bei elekezi ya kuunganisha maji ili kutengeneza usawa katika eneo hilo limekuwa na malalamiko kutoka kwa wateja wanaotaka kuunganishiwa maji.
Agizo hilo alilitoa juzi, wakati wa mkutano uliowahusisha wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani uliolenga kujadili hali ya upatikanaji wa maji na miradi inayoendelea kutekelezwa katika mikoa hiyo chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Dar es Salaam (Dawasa).
Aweso alisema kitendo cha kuwa na gharama tofauti za kuunganisha maji kinazua maswali na kuashiria kuna michezo isiyofaa inafanyika.
“Kama kuna jambo ambalo nataka lifanyike kwa haraka ni kuwa na bei elekezi ya kuunganishiwa maji haiwezekani mtu anaunganishiwa maji kilomita tano halafu bei zinakuwa tofauti. Hii inaleta mashaka kwanini kusiwe na bei tofauti, sasa hivi wafanyakazi wanachagua kwenda kitengo cha maunganisho kuna nini huko kama sio upigaji.
“Nataka eneo hilo lisimamiwe kikamilifu ili kufikia lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani lazima tuthibiti vitu hivi vinavyowaweka wananchi katika wakati mgumu,”alisema Aweso.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala alisema kazi kubwa imefanyika katika kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa na maji ya kutosha ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo nyuma.
“Upotevu wa maji ulikuwa asilimia 56 yani mnahangaika kuongeza upatikanaji wa maji halafu mengi yanapotea.Ilifika mahali hata dawa ya kuweka kwenye maji haikuwepo, tulikuwa na madeni makubwa ya wazabuni,”.
Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema, wamejipanga kuhakikisha wanamaliza tatizo la uhaba wa maji na kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuondoa changamoto ya maji nchini.
Comments
Post a Comment