WAZIRI MKUU ASISITIZA UADILIFU UJENZI MJI WA SERIKALI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali wahakikishe wanazingatia uadilifu katika matumizi ya fedha ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara zote ambazo baadhi ya watumishi wake wake bado wako Dar Es Salaam wahakikishe wanahamia Dodoma kama ilivyoelekezwa na Serikali. “ Simamieni agizo hili kikamilifu.”
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Septemba 5, 2022) wakati akizungumza baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ujenzi wa Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma, ambapo amewashukuru na kuwapongeza wakandarasi wanaojenga mji huo.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ujenzi wa Makao Makuu unaendelea vizuri ni nzuri na lazima tujivunie maono ya viongozi na kazi nzuri wanayoifanya pamoja na kazi nzuri za wataalamu wetu.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa mji wa Serikali utakuwa wa kisasa kwa kuwa utaendeshwa kidijitali “fedha za kutekeleza haya zipo na ninawahakikishia kila kitu kitakamilika, dhamira ya Rais Mheshimiwa Samia ni kufanya makao makuu kuwa bora zaidi.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi katika mradi huo waendelee kufanyakazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na waendelee kuzingatia maelekezo wanayopewa viongozi wao ili wawe na uwezo wa kujenga na kusimamia kazi zao.
Comments
Post a Comment