SPIKA TULIA AIPONGEZA BENKI YA NBC KUBORESHA SEKTA YA KILIMO
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Ackson ameguswa na kupongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika kuboresha sekta ya kilimo hapa nchini kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa wadau wa sekta hiyo muhimu.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonyesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya, Dk. Tulia alionyesha kuvutiwa zaidi na huduma ya Bima ya Kilimo inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Jubilee Insurance ikilenga kuwalinda wakulima, wavuvi na wafugaji nchini dhidi ya hasara pindi wanapopata majanga mbalimbali yanayoweza kuathiri uzalishaji wao.
“Pamoja na huduma zote nzuri mnazozitoa benki ya NBC kwa wakulima nimevutiwa sana na huduma ya Bima ya kilimo kwa wakulima. Nimevutiwa zaidi baada ya kusikia tayari kuna wakulima wa tumbaku huko mkoani Tabora wameshanufaika na huduma hii. Hiki ni kithibitisho tosha kuwa huduma hii inatekelezeka vizuri kwa faida ya wakulima wetu…hongereni sana kwa kuonesha njia,’’ amepongeza.
Mbali na huduma hiyo, akiwa kwenye banda la benki hiyo Dk. Tulia alipata wasaa wa kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kupitia mkakati mkubwa wa benki hiyo unaolenga kuinua sekta ya kilimo nchini unaofahamika kama ‘NBC Shambani’ unaohusisha mnyororo wote wa sekta ya kilimo kuanzia kwa mkulima, mchakataji wa mazao ya kilimo hadi msambazaji.
Comments
Post a Comment