NAIBU WAZIRI MWAKIBETE ATOA WIKI MBILI BANDARI YA KAREMA KUANZA KUTOA HUDUMA.



Naibu Waziri Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa wiki mbili kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha bandari mpya ya Karema inaanza kutoa huduma ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa nchi ya Tanzania kupitia mkoa wa Katavi na Nchi Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo mkoani humo ambao
umekamilika kwa asilimia mia moja Naibu Waziri Mwakibete amesema
kukamilika na kutoa hudma kwa bandari hiyo iliyogharimiwa na Serikali kwa fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni 30 kutachochea uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.

"Fedha nyingi zilizowekwa hapa lazima zianze kutumika vitu vilivyobaki ni
vichache sana na viko ndani ya uwezo wetu hivyo tuvikamilishe haraka na
tuanze kutoa huduma muda hausubiri na mradi umeshakamilika. Amesisitiza
Naibu Waziri Mwakibete.


Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na mradi huo Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 inaendelea na ukarabati wa meli ya MT. Sangara na
imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya mbili za abiria na mizigo
zitakazotoa huduma katika bandari za ziwa Tanganyika na na Nchi za jirani.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewataka TPA kuhakikisha wananchi wa Kata ya Karema wanapewa kipaumbele cha ajira hususani kwa kazi
zisizohitaji utaalam sababu ajira hizo zitachochea uchumi wao pia walinzi wa
miundombinu hiyo ili iweze kudumu.



Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika ametumia fursa hiyo kuwataka
wananchi kuunda vikundi vidogo vidogo ili kutumia fursa ya uwepo wa mradi
huo mkubwa kupata ajira za muda mfupi na mrefu wakati itakapoanza
kufanya kazi.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward
Mabula amesema mradi kwa sasa umeshakamilika na kumuhakikisha NaibuWaziri kuwa kazi zilizobaki ni kufunga umeme kazi itakayofanyika kwa wiki
moja pamoja na uletaji wa mitambo ya kuhudumia mizigo.


"Mhe. Naibu Waziri huduma hapa itaanza wakati wowote sababu baada ya
kuunganisha umeme, tutafanya majaribio kwa siku chache na baadae
tutakamilisha taratibu za uendeshaji na tutaanza kutoa huduma" amesema
Kaimu Meneja Edward Mabula.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mwakibete yuko Mkoani Katavi kwa ziara ya siku
mbili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Wizara ya
Ujenzi na Uchukuzi.

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

Comments